Mambo Manne Yaliyochangia Anguko la Shule za Vipaji Katika Matokeo Ya Mtihani wa Kidato cha Nne

21:19


Anguko la shule za sekondari za Serikali zikiwamo za vipaji maalumu katika matokeo ya mtihani wa kidato cha nne, limedaiwa kusababishwa na walimu kukata tamaa, miundombinu duni na mazingira magumu ya kufundishia na kusomea.

Shule za vipaji maalumu, zinazochukua wanafunzi wanaofanya vizuri katika mtihani wa darasa la saba, hazimo kwenye orodha ya shule 50 bora, na kati yao ya kwanza inashika nafasi ya 53.

Orodha hiyo imetawaliwa na shule binafsi na za taasisi zisizo za serikali, hasa za kidini wakati za Serikali zinapambana kuanzia nafasi ya 53.

Kukata tamaa kwa walimu na mazingira magumu ya kufundishia ndiko kumeelezwa na wachambuzi mbalimbali kuwa ndiyo sababu kuu ya kuporomoka kwa kiwango cha ufaulu kwa shule hizo.

Katibu Mtendaji wa Necta, Dk Charles Msonde alitaja shule 10 bora juzi kuwa ni Kaizirege ya Kagera, Alliance Girls (Mwanza), St Francis Girls (Mbeya), Alliance Boys (Mwanza), Canossa (Dar es Salaam), na Marian Boys (Pwani).

Nyingine ni Alliance Rock Army (Mwanza), Fedha Girls (Dar es Salaam), Feza Boys (Dar es Salaam) na Uru Seminary (Kilimanjaro).

Huu ni mwaka wa tatu mfululizo kwa Kaizirege kuongoza katika mitihani ya kitaifa huku Alliance Boy na Girls zikiwamo pia katika 10 bora kwa miaka mitatu mfululizo.
 Anguko la shule za Serikali 
Kuanguka kwa shule hizo kumedhihirika juzi mara baada ya kutangazwa kwa matokeo ya kidato cha nne ambayo sehemu kubwa hazikufanya vizuri.

Dk Msonde alizitaja baadhi ya shule za sekondari za vipaji maalumu kuwa ni Ilboru ambayo imeshika nafasi ya 53, Kibaha (69), Kilakala (94), Mzumbe (71), Tabora Boys (124), Tabora Girls (128) na Msalato (148).

Akizungumzia hatua hiyo, Meneja wa Utafiti na Sera wa Taasisi ya Hakielimu, Godfrey Boniventure alisema anguko hilo linaonyesha wazi kuwapo kwa tabaka kubwa kati ya walionacho na wasio nacho.

“Shule zote 10 za mwisho ni za Serikali ambazo wanasoma watoto wa maskini. Kibaya zaidi hata za vipaji maalumu zilizokuwa zikitegemewa zipo hoi. Hii ni hatari kwa Taifa,” alisema.

Alisema tabaka hilo litawafanya watoto wanaotoka kwenye familia zenye uwezo kupata nafasi za juu kwenye soko la ajira, huku maskini wakishindwa kuingia kwenye ushindani huo.

Profesa wa Chuo Kikuu Ruaha (RUCU), Gaudence Mpangala alisema anguko hilo limechangiwa kwa kiasi kikubwa na kukata tamaa kwa walimu.

Alisema walimu hawana moyo wa kuendelea kufanya kazi hiyo na utafiti kwenye baadhi ya shule unaonyesha wengi wao wanaingia darasani kukamilisha ratiba na si kufundisha.

Profesa Mpangala alisema sababu iliyowafanya kufikia hatua hiyo ni Serikali kutowalipa stahiki zao kama mishahara, motisha, makato na mazingira magumu ya kufundishia.

“Ilitokea kwangu. Niliamua kumhamisha mwanangu aliyekuwa akisoma shule ya vipaji maalumu kwa sababu walikuwa hawaingii darasani, sikuwalaumu hata kidogo, niliona wazi mazingira yao ya kazi ni magumu.”

Alisema sera ya elimu bure itachangia anguko kubwa zaidi kutokana na hali ya shule hizo kuendelea kuwa mbaya. “Majengo ya shule za vipaji maalumu yamechoka, Serikali haipeleki pesa na wazazi hawachangii. Kitakachotokea hapo ni kufeli zaidi,” alisema.

Profesa wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Kitila Mkumbo alisema kukata tamaa kwa walimu kunachangia shule hizo kufanya vibaya.

Aliitaka Serikali kurejesha hadhi ya shule zake ili ziendelee kuwa kimbilio la wanyonge.

“Ari ya walimu kufundisha imeshuka kwa kiwango kikubwa, Serikali isipotoa kipaumbele kwa kundi hili, itakuwa hatari zaidi,” alisema.

Ilboru wanena 
Mwalimu Mkuu wa Shule ya Sekondari ya Ilboru, Julius Shura alikiri kuwa hali ya shule hiyo ni taabani kutokana na kuchakaa kwa miundombinu.

“Hata hivyo, tumejitahidi kutoa wanafunzi wawili bora ambao wametokana na jitihada zetu walimu licha ya kuwa mazingira ya kufundishia ni magumu. Tunaomba Serikali itupie jicho shule hizi ambazo zilikuwa taa kwa watoto wa Kitanzania wenye vipaji maalumu,” alisema.

“Hali ni ngumu zaidi kwa watoto wenye ulemavu, hakuna mazingira rafiki hata kidogo. Piga picha bajeti ya Sh1,500 kwa mtoto anayesoma sayansi ni ndogo sana kwa siku, usitegemee kwamba atafanya maajabu,” alisema.

Siri ya shule binafsi kuongoza 
Katibu Mkuu wa Shirikisho la Wamiliki na Mameneja wa Shule na Vyuo Visivyo Vya Serikali (Tamangsco), Benjamin Nkonya alisema siri ya shule zao kuongoza ni kuwekeza kwa walimu.

“Tunawasikiliza walimu, kuwapa heshima wanayostahili na kuhakikisha wanapatiwa kila wanachohitaji kama mikopo ya magari na nyumba, ukimjali mwalimu mengine yote yatakwenda vizuri,” alisema.

You Might Also Like

0 comments

Popular Posts

Like us on Facebook

Flickr Images